Polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaomtaka rais Joseph Kabila aondoke madarakani.
Watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wamekamatwa, wakiwemo waandishi habari.
Maafisa wamepiga marufuku maandamano hayo na huduma za intaneti zimefungwa.
Kanisa katoliki limewataka raia washirika katika maandamano ya amani baada ya misa ya Jumapili - wakibeba bibilia rosari na misalaba.
Maafisa wa usalama walikabiliana na maandamano hayo kwa kutumia nguvu katika miji tofuati nchini.
Katika mji mkuu Kinshasa, walinda amani wa Umoja wa mataifa wanaarifiwa kutawanywa kujaribu kuwatenganisha waandamanji na vikosi vya usalama nchini.
Kumeshuhudiwa maandamano mengi dhidi ya rais Kabila tangu muhula wake umalizike zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Congo inakabiliwa pia na mizozo kadhaa ya makundi ya kujihami, husuan katika maeneo ya mashariki na kati mwa nchi hiyo.
Mwendelezo: Watano wafariki
Jeshi la Kongo (DRC) limewaua waandamanaji watano na wengine 17 kujeruhiwa kufuatia maandamano makubwa ya kupinga Rais Kabila kuendelea kuwa madarakani. Maandamano hayo yaliitishwa na kanisa Katoliki nchini humo. Kabila amegoma kung'atuka tangu mhula wake uishe disemba 2016.
Kabila amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 na mamlaka yake yaliisha rasmi mwaka 2016.
Kwenye makubaliano yaliyoratibiwa na Kanisa Katoliki aliruhusiwa kuendelea kubaki madarakani na kuitisha uchaguzi mwaka 2017 lakini serikali yake imesema uchaguzi mpya ni hadi Disemba 2018