Madereva wawili wa mabasi yaendayo mikoani wamekamatwa

Madereva wawili wa mabasi yaendayo mikoani wamekamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kurekodiwa video wakilipita lori kwa namna ambavyo ingeweza kusababisha ajali.
Madereva hao ni wa basi la New Force linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Kyela mkoani Mbeya na Galaxy Classic linaloelekea mkoani Njombe.
Mapema wiki hii video inayoonyesha mabasi yakilipita lori kulia na kushoto kwa pamoja ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii lakini baada ya muda video nyingine iliwaonyesha madereva hao wakiwa wamefungwa pingu mbele ya mabasi yao.
Kwenye video ya kwanza, New Force linaonekana likipita upande wa kulia wa lori na Galaxy Classic likipita upande wa kushoto wa lori hilo hilo, kwa pamoja.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Mchemba, aliwapongeza wananchi waliotoa taarifa za mabasi hayo zilizosaidia kukamatwa kwao.
Kupitia ukurasa wake wa Istagram juzi, Mwigulu aliandika, "Madereva wa magari madogo au makubwa kumbukeni mmebeba dhamana ya maisha ya watu mliowabeba kwenye magari au wanaotembea kwa miguu."Image may contain: outdoor
Aidha, Mwigulu alisema mtu yeyote anayehatarisha maisha ya watu hataachwa na atakamatwa na kuchukuliwa hatua popote atakapopatikana.
"Asanteni kwa mliotupa ushirikiano kuonyesha ile video ya mabasi mawili yaliyokuwa yakishindana kulipita lori kwa njia ambayo ingesababisha ajali na hakukuwa na tahadhari yoyote iliyochukuliwa," aliandika zaidi.
Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Fortunatus Muslim, aliliambia Nipashe kuwa wameshafungia leseni za madereva hao kwa kipindi cha miezi sita.
"Kwa mamlaka niliyonayo kwa mujibu wa sheria tayari nimewachukulia hatua ya kufungia madaraja yao ya leseni hivyo hawataruhusiwa kuendesha mabasi ya abiria kwa kipindi cha miezi sita, wakati wakisubiri hukumu ya mahakama," alisema Kamanda Muslim.
Alisema hatua ya kwanza waliyochukua ni kuwakamata na kuwasafirisha kutoka Kyela mkoani Mbeya na Njombe walipokuwa wanaelekea na kuwarudisha Makambako ambako walitenda tukio hilo.
"Tulipoona tu ile clip ya video tuliagiza askari wetu wawakamate baada ya kufika mwisho wa safari na jana (juzi) walisafirishwa kuelekea Makambako ambako walitendea kosa hilo," alisema Kamanda Muslim.
Alisema wakiwa hapo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kukamilisha upelelezi kabla ya kufikishwa mahakamani.
Muslim pia aliwataka madereva wengine nchini kufuata taratibu na sheria za usalama barabarani na kwamba Jeshi la Polisi halitawafumbia macho wanaozikiuka.
"Vitendo vya kihuni na hatari havivumiliki," alisema Kamanda Musilimu. "Haiwezekani madereva wawili wa mabasi walipite lori kwa wakati mmoja na wakati huo lori la mafuta lilikuwa linakuja mbele".
"Ingeweza kutokea ajali kubwa na kusababisha madhara kwa watu na mali zao."