Mgombea ubunge wa kinondoni kupitia CHADEMA, Salum Mwalimu amemwekea mapingamizi matano mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM Maulid Mtulia.
Lakini saa chache kabla ya kuanza kampeni, Mwalimu aliwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM, akiwa na hoja tano, ikiwemo ya kutofanya mrejesho wa gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakili wake, Frederick Kihwelo aliliambia Mwananchi kuwa kwanza, Mtulia hajafanya mrejesho wa gharama za uchaguzi wa mwaka 2015, alipogombea kwa tiketi ya CUF.
“Jambo hili hufanywa na mtu yeyote aliyegombea nafasi ya udiwani, ubunge na urais na haijalishi kama alishinda au kushindwa,” alisema Kihwelo.
“Unapaswa kuandaa mchanganuo wa gharama zako za uchaguzi na kuzipeleka ofisi ya NEC.”
Alisema hoja ya pili ni Mtulia kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria kwa kutojaza kwa usahihi fomu zake, kwa madai kuwa zimepigwa muhuri wa katibu wa CCM badala ya muhuri wa chama hicho tawala.
“Muhuli ulipigwa katika fomu yake unasomeka wa katibu wa chama badala ya muhuri wa chama. Hii inaonyesha chama hakijamthibitisha kugombea. Jambo hili liliwasumbua sana Chadema mwaka 2014 kwa baadhi ya wagombea wao kuenguliwa, ” alisema Kihwelo.
Alisema hoja ya mwisho ni Mtulia kujaza fomu akieleza kuwa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, jambo ambalo Kihwelo amesema si kweli.
“Hiki kilimo cha mbogamboga amekianza lini kwa sababu tunajua alikuwa mbunge. Tunamtaka athibitishe hili,” alisema.
Mwananchi lilipomtafuta Mtulia kujibu hoja hizo alijibu kwa kujiamini kuwa “hili jambo ni jepesi sana na nimeandika ninachokijua na hakuna pingamizi hapo”.
Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Latifa Almasi alisema wamepokea mapingamizi lakini haweka wazi idadi yake, na kubainisha kuwa leo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Aron Kagurumjuli, atayatolea ufafanuzi.
Chanzo: Mwananchi