Msafara wa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole wapata ajali

Msafara wa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Hamphrey Polepole umepata ajali katika eneo la Kijiji cha Nyamidato, Kata ya Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Vx yenye namba za usajili T150 CWE iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina moja la Kibuta wakati wakielekea katika ziara ya kiongozi huyo wilayani Kakonko, mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma ACP Martin Otieno amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza chanzo cha ajali hiyo kuwa ni kupasuka kwa gurudumu la nyuma upande wa kulia.

Kwa mujibu wa Kamanda Otieno, waliojeruhiwa ni pamoja na Katibu wa CCM mkoa Naomi Kapambala, Mwenyekiti wa UVCCM Sylivia Sigura pamoja na Katibu Mwenezi, Feruz ambao wamekimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Kibondo kwa matibabu.
Gari lililopinduka - Toyota Landcruiser V8

Polepole amewasili leo mkoani Kigoma na kupokelewa wilayani Uvinza akitokea mkoani Tabora ambapo atakuwa Kigoma kwa takribani siku tatu.